Wednesday, 27 December 2006

Mwaka Mpya Ulimwengu Mpya!

Kama ilivyo desturi yetu tunapoanza mwaka mpya, mara nyingi wengi wetu huanza mwaka kwa maneno yanayosema "mwaka mpya na mambo mapya". Lakini maneno haya huwa hayana maana yoyote endapo hatutafanya tathmini ya yaliyofanyika mwaka uliopita na kuwa na malengo madhubuti kwa mwaka unaofuata. Wengine wetu huishia kusema tu tusahau yaliyopita na tugange yajayo bila hata kujiuliza ni yapi hayo yaliyopita, ni wapi tulikosea ili kusudi tusije rudia makosa yale yale na nini cha kufanya kwa mwaka unaofuata katika kuleta maendeleo binafsi na jamii nzima inayotuzunguka na kuepelekea mabadaliko duniani kote.

Binafsi ninaungana mkono na kauli mbiu ya serikali ya Mheshimiwa Rais wetu, Jakaya Mrisho Kikwete kwa kauli mbiu yake "Nguvu Mpya, Kasi Mpya na Mambo Mapya" lakini kama nilivyokwisha kusema hapo juu kwamba bila kutambua kwa hakika ni mambo gani hayo mapya tunayaongelea au kuyapa kipaumbele, kwa kweli kauli mbiu hii inaweza kuwa sawa na maneno matupu!

Ni furaha yangu kutambulikana kidunia kwa kazi tunayoifanya sisi wanablogu ya kuielimisha dunia kwa njia ya teknolojia mpaka kuchaguliwa na gazeti la TIME kama "Person of the Year", hivyo basi ni jukumu letu kuendeleza kazi hii nzuri katika kufanya mabadiliko duniani. Ombi langu kwenu nyote ni kwamba tuendelee kuitumia njia hii katika kuleta AMANI duniani, kuondoa UMASKINI na zaidi kuzidi kuelimishana.

Na kauli mbiu yetu iwe;
"Mwaka Mpya, Nguvu Mpya, Kasi Mpya na Mambo Mapya-Pamoja Daima"

No comments: