Friday, 29 December 2006

Heka heka za mgao wa umeme!

"Mgao wa umeme sasa basi" haya ndiyo maneno yanayosikika na watanzania kwa sasa ukiuliza juu ya swala la mgao wa umeme! Tatizo hili limekuwa sugu kwa muda mrefu sasa na sina hakika kama suluhisho la kudumu limepatikana au ni baraka ya mvua ambazo zimeendelea kunyesha siku mbili tatu, au labda tuseme swala la tatizo la umeme nchini ni sawa na dondandugu/ kidonda kisichopona! Hilo nawaachiwa wenzi wangu tuendelee kulijadili kwa pamoja.

Katika kipindi cha pilika pilika za mgao wa umeme ambacho kimeleta malumbano mengi mimi nimejifunza jambo moja muhimu. Kipindi hiki kigumu kimepelekea baadhi wa watanzania kulazimika kufanya baadhi ya shughuli zao usiku ili kukabiliana na tatizo hili, baadhi ya shughuli ambazo zimekuwa zikifanyika usiku si mchana kama ilivyozoeleka ni pamoja na shughuli na kuchomelea vyuma, mashine za kusaga unga na shughuli nyinginezo na kwa wengine wafanyao kazi maofisini labda kwao kipindi hiki kilikuwa ni cha neema ya kupokea ujira bila uzalishaji wowote.

Binafsi na kwa wale waliopata kuishi ughaibuni hasa nchi za magharibini tutakubaliana kwamba utamaduni au desturi ya kufanya kazi usiku na mchana ni jambo la kawaida. Kwa nchi kama Uingereza makampuni mengi ya uzalishaji na hata ya kutoa huduma hufanya kazi masaa 24 kwa siku, siku 7 kwa wiki katika siku zote 365 za kila mwaka. Mfano wa makumpuni hayo ni kama Tesco, Waitrose, WHSmith, Royal Mail na makampuni mengine mengi mno. Hata shughuli za ujenzi au marekebisho ya mabarabara makuu (Motorways) au reli hufanyika usiku wa manane au siku za wikiendi. Shirika kama la Royal Mail ambalo hushughulika na usambazaji wa barua na vifurushi hufungwa masaa kadhaa tu katika mwaka yaani siku ya tarehe 25 Desemba ya kila mwaka.

Mtazamo wangu ni kwamba kama tutaendelea na utamaduni huu ambao tulilazimika kuufuata wakati wa heka heka za mgao wa umeme labda itasadia kasi ya maendeleo ya nchi yetu na pia kuongeza ajira na pengine kupunguza hata kasi ya wimbi la ujambazi na ujangili ambao umekuwa ukilitikisa taifa letu changa. Nafikiri wezi na majambazi ambao hufanya vitendo hivyo vya katili nyakati za usiku kama wangelikuwa na shughuli halali za kufanya kuwaingizia kipato nyakati hizo pengine wangefanya hizo kazi za uzalishaji ama utoaji huduma.

Labda tu ombi kwa serikali liwe ni kuwaongezea ujira na idadi askari polisi wa usalama kutokana na kodi itakayopatikana kutokana na ongezeko la uzalishaji mali.

Ni mtazamo binafsi!

Thursday, 28 December 2006

Watanzania Waishio Uingereza!

Watanzania waishio nchini Uingereza wameshauriwa kurudi nyumbani Tanzania kuisadia serikali ya awamu ya nne kuendelza nchini. Maneno hayo yalisemwa na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza Mama Maajar.

Balozi wa Tanzania nchini Uingereza Mama Maajar amewashauri watanzania wasomi waishio Uingereza kurudi nyumbani kusaidia kuleta maendeleo ya nchi badala ya kubakia kuilalamikia serikali kila mara juu ya hili na lile. Mama Maajar aliyasema hayo alipokutana na watanzania jijini London kuwasalimia na kujitambulisha kwao wiki chache zilizopita. Mama Maajar aliwataka watanzania hao wajiulize ni nini wataifanyia nchi yao na si nchi itawafanyia nini!

Takwimu zinaonyesha kwamba katika wantanzania elfu tano(5,000) wasomi waishio Uingereza ni asilimia tano (5%) tu kati ya hao wanaofanya kazi zinazoendana na taaluma zao na waliobaki yaani asilimia tisini na tano (95%) hufanya vibarua tu (unskilled labour) ili kuweza kusukumana na hali ngumu ya maisha hapa nchini Uingereza.

Katika kipindi cha miaka mitano hadi kumi iliyopita watanzania wengi waliongia nchini Uingereza aidha kwa ajili ya kujiendeleza kimasomo, matembezi ama kikazi walitawaliwa na mawazo duni kwamba wamefika peponi na mawazo ya kurudi Tanzania kwao ilikuwa ni ndoto. Huu tunaweza kuuita ni ulimbukeni. Lakini hali ni tofauti kwa miaka ya sasa ambapo wimbi la watanzania kurudi nyumbani tanzania limeongezeka mno. Hali hii inaweza kuwa ni kutokana na kasi ya maendeleo kidunia, lakini pia tatizo kubwa limekuwa ni swala zima la muungano wa nchi za ulaya. Mmiminiko wa waulaya mashariki nchini Uingereza umeleta mfakarakano mkubwa sana na ongezeko la ugumu wa maisha.

Kwa wale ambao bado hawajajiwekea mipango madhubuti ya kujiandaa kurudi nyumbani katika kipindi cha miaka miwili mitatu ijayo wakifiri kwamba hapa ndiyo nyumbani ni wazi kwamba wanajidanganya nafsi zao.

Wazaramo wanasema ,"Ukae kunoga"

Wednesday, 27 December 2006

Mwaka Mpya Ulimwengu Mpya!

Kama ilivyo desturi yetu tunapoanza mwaka mpya, mara nyingi wengi wetu huanza mwaka kwa maneno yanayosema "mwaka mpya na mambo mapya". Lakini maneno haya huwa hayana maana yoyote endapo hatutafanya tathmini ya yaliyofanyika mwaka uliopita na kuwa na malengo madhubuti kwa mwaka unaofuata. Wengine wetu huishia kusema tu tusahau yaliyopita na tugange yajayo bila hata kujiuliza ni yapi hayo yaliyopita, ni wapi tulikosea ili kusudi tusije rudia makosa yale yale na nini cha kufanya kwa mwaka unaofuata katika kuleta maendeleo binafsi na jamii nzima inayotuzunguka na kuepelekea mabadaliko duniani kote.

Binafsi ninaungana mkono na kauli mbiu ya serikali ya Mheshimiwa Rais wetu, Jakaya Mrisho Kikwete kwa kauli mbiu yake "Nguvu Mpya, Kasi Mpya na Mambo Mapya" lakini kama nilivyokwisha kusema hapo juu kwamba bila kutambua kwa hakika ni mambo gani hayo mapya tunayaongelea au kuyapa kipaumbele, kwa kweli kauli mbiu hii inaweza kuwa sawa na maneno matupu!

Ni furaha yangu kutambulikana kidunia kwa kazi tunayoifanya sisi wanablogu ya kuielimisha dunia kwa njia ya teknolojia mpaka kuchaguliwa na gazeti la TIME kama "Person of the Year", hivyo basi ni jukumu letu kuendeleza kazi hii nzuri katika kufanya mabadiliko duniani. Ombi langu kwenu nyote ni kwamba tuendelee kuitumia njia hii katika kuleta AMANI duniani, kuondoa UMASKINI na zaidi kuzidi kuelimishana.

Na kauli mbiu yetu iwe;
"Mwaka Mpya, Nguvu Mpya, Kasi Mpya na Mambo Mapya-Pamoja Daima"