Monday, 19 February 2007
Barua ya wazi kwa Mh.Rais Jakaya Mrisho Kikwete
Mh. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ndugu Jakaya Mrisho Kikwete, ifuatayo ni barua ya wazi kwako kuelezea hali halisi ya wanyama pori katika baadhi ya mbuga zetu za wanyama nchini Tanzania. Swala hili lilikuwa liwasilishwe kwako siku ulipokutana na watanzania waishio nchini Uingereza katika kipindi cha maswali na majibu, lakini kutoka na uhaba wa muda haikuwezekana hivyo basi kutokana na maendeleo ya sayansi na tekinolojia ya dunia ya sasa imefikirika labda kwa njia hii bado itasaidia kufikisha ujumbe huu kwako.
Mh. Rais, itakumbukwa kwamba hivi karibuni Tanzania imetangazwa kuwa ni nchi moja wapo katika zile nchi zenye rekodi ya kuwa na Maajabu Saba ya Dunia(Seven Wonders of The World) kutokana na uhamaji wa mamilioni ya wanyama aina ya nyumbu(kama sijakosea) kila mwaka toka mbuga za Serengeti wakivuka mto Mara na kurudi tena kutokana na tofauti ya vipindi vya majira ya hali ya hewa, ama kwa hakika jambo hili ni la kihistoria na ni jambo la kujivunia mno.
Lakini si hilo tu kwani pia unapoongelea bara la Afrika, ukitazama ramani(Atlasi) ya Dunia, nomino/jina Tanzania si geni kabisa katika kuelezea vielelezo kadha wa kadha juu ya la Bara hili, kwa mfano unapoongelea sehemu ya juu kabisa ya mwinuko(highest peak) katika bara zima la Afrika ni lazima uitaje Tanzania, kwa maana mlima wa Kilimanjaro ndiyo mlima mrefu kuliko yote barani Afrika, tena unapotaka kuongelea kina kirefu zaidi barani Afrika utaongelea ziwa Tanganyika ambalo limepitiwa na bonde la Ufa(Rift Valley) hivyo basi ni lazima uitaje nchi ya Tanzania ambayo kwayo ziwa Tanganyika ndiyo kiini cha jina Tanzania. Unapokuja kuongelea ziwa kubwa kuliko yote barani Afrika yaani ziwa Victoria, ni wazi kwamba utakuwa unaikosea Tanzania usipoitaja kwa maana sehemu kubwa ya ziwa hili iko upande wa Tanzania tukushiriki pamoja na majirani zetu nchi za Kenya na Uganda na bila kusahau pia kwamba hapo awali chanzo cha mto Nile ambao ni mto mrefu kuliko yote barani Afrika, kilijulikana kuwa ni ziwa Victoria, Victoria = Tanzania, ambavyo ni tofauti hivi sasa.
Licha ya yote hayo Tanzania inajulikana kuwa na madini yapatikanayo nchini Tanzania pekee si kwa Afrika tu bali Duniani kote, madini ya TANZANITE.
Na kwa kumbukumbu za kihistoria itakumbukwa kwamba fuvu la kichwa cha mtu ambaye anasemekana alikuwa wa kwanza kuishi Duniani lilipatikana Tanzania, fuvu la "Zinjanithropas",sina hakika wanasayansi wameshagundua lipi kwa sasa.
Kwa kifupi ni kwamba Tanzania imekuwa kwenye ramani ya Dunia na katika Historia kwa muda mrefu sasa, ingawaje utangazwaji wake umekuwa hafifu.
Miaka ya hivi karibuni ambapo Tanzania imekuwa ikiianza kujitangaza kwa kasi mpya,nguvu mpya na ari mpya hasa kupitia swala la utarii, ieleweke wazi kwamba majivuno haya huenda yakawa ni ya muda mfupi tu pengine kipindi cha miaka kumi(10) mpaka labda ishirini(20) hivi. Hii ni kutokana na hali ilivyo huko mbugani.
Mh. Rais, ukweli ni kwamba hali halisi ya Uvunaji wa Wanyama Pori katika mbuga zetu unafanyika kiholela sana na kama hali hii itaendelea hivi tusijepigwa na bumbuwazi katika kipindi cha miaka iliyoelezewa hapo juu baadhi ya wanyama katika mbuga zetu wakawa wametoweka kabisa, mbaya zaidi baadhi ya wanyama hao huwenda ikawa na ile ya wanyama ambao wamekuwa ni kivutio zaidi, wanyama ambao wamewekwa kwenye orodha iliyopewa jina la "The Big Five", mfano wanyama kama Simba(mfalme wa Nyika), ambapo wanyama kama hawa wanapatikana kwenye nchi chache Afrika moja wapo ikiwa ni Tanzania.
Huvunaji huu wa wanyama wa kiholela ambao unaendana na uchukuzi wa takwimu za idadi ya wanyama kiholela yaani kwa makisio ama makadirio tu ambao sio sahihi unaoambatana na rushwa iliyokithiri, ukiendelea kufumbiwa macho ama usipovaliwa njuga itabaki kuwa historia kwa vizazi vijavyo kwamba Tanzania ilikuwa na hiki na kile na pengne watoto wetu na wajukuu itawapasa kwenda nchi nyingine kuona yale tuliokuwa tunajivunia nayo watanzania tena kwa gharama kubwa mno na wengine kushindwa kufanya hivyo kabisa.
Mh. Rais ni haya machache tu ambayo ningependa kuwasilisha kwako!
Wako mtiifu katika Ujenzi wa Taifa la Tanzania
Mtanzania Mzalendo!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment