Friday 29 December 2006

Heka heka za mgao wa umeme!

"Mgao wa umeme sasa basi" haya ndiyo maneno yanayosikika na watanzania kwa sasa ukiuliza juu ya swala la mgao wa umeme! Tatizo hili limekuwa sugu kwa muda mrefu sasa na sina hakika kama suluhisho la kudumu limepatikana au ni baraka ya mvua ambazo zimeendelea kunyesha siku mbili tatu, au labda tuseme swala la tatizo la umeme nchini ni sawa na dondandugu/ kidonda kisichopona! Hilo nawaachiwa wenzi wangu tuendelee kulijadili kwa pamoja.

Katika kipindi cha pilika pilika za mgao wa umeme ambacho kimeleta malumbano mengi mimi nimejifunza jambo moja muhimu. Kipindi hiki kigumu kimepelekea baadhi wa watanzania kulazimika kufanya baadhi ya shughuli zao usiku ili kukabiliana na tatizo hili, baadhi ya shughuli ambazo zimekuwa zikifanyika usiku si mchana kama ilivyozoeleka ni pamoja na shughuli na kuchomelea vyuma, mashine za kusaga unga na shughuli nyinginezo na kwa wengine wafanyao kazi maofisini labda kwao kipindi hiki kilikuwa ni cha neema ya kupokea ujira bila uzalishaji wowote.

Binafsi na kwa wale waliopata kuishi ughaibuni hasa nchi za magharibini tutakubaliana kwamba utamaduni au desturi ya kufanya kazi usiku na mchana ni jambo la kawaida. Kwa nchi kama Uingereza makampuni mengi ya uzalishaji na hata ya kutoa huduma hufanya kazi masaa 24 kwa siku, siku 7 kwa wiki katika siku zote 365 za kila mwaka. Mfano wa makumpuni hayo ni kama Tesco, Waitrose, WHSmith, Royal Mail na makampuni mengine mengi mno. Hata shughuli za ujenzi au marekebisho ya mabarabara makuu (Motorways) au reli hufanyika usiku wa manane au siku za wikiendi. Shirika kama la Royal Mail ambalo hushughulika na usambazaji wa barua na vifurushi hufungwa masaa kadhaa tu katika mwaka yaani siku ya tarehe 25 Desemba ya kila mwaka.

Mtazamo wangu ni kwamba kama tutaendelea na utamaduni huu ambao tulilazimika kuufuata wakati wa heka heka za mgao wa umeme labda itasadia kasi ya maendeleo ya nchi yetu na pia kuongeza ajira na pengine kupunguza hata kasi ya wimbi la ujambazi na ujangili ambao umekuwa ukilitikisa taifa letu changa. Nafikiri wezi na majambazi ambao hufanya vitendo hivyo vya katili nyakati za usiku kama wangelikuwa na shughuli halali za kufanya kuwaingizia kipato nyakati hizo pengine wangefanya hizo kazi za uzalishaji ama utoaji huduma.

Labda tu ombi kwa serikali liwe ni kuwaongezea ujira na idadi askari polisi wa usalama kutokana na kodi itakayopatikana kutokana na ongezeko la uzalishaji mali.

Ni mtazamo binafsi!

No comments: