Thursday 18 January 2007

CCM London wakutana na M/Kiti Taifa CCM

Wanachama wapya na wale wa zamani wa CCM tawi la London wakutana na M/kiti Taifa Mh. J.K. Halfa hiyo iliyofanyika katika Hotel aliyofikia Mh.Rais ambapo ndipo Mh. alikutana na watanzania waishio UK siku ya jumapili ya tarehe 14 Jan 2007, ni Hoteel ya Churchill katikati ya mji wa London.

Hafla hiyo fupi iliyoandaliwa na wana CCM-London, ilifunguliwa na Katibu wa Muda wa Tawi hilo ndugu Mpopo ambaye alimkaribisha M/kiti wa muda wa tawi Nd. Sharif Maajar ambaye alisoma risala fupi kwa Mh. Rais. Naye Mh.Rais ambaye ndiye m/kiti taifa CCM aliongea machache na kuwashukuru wale wote walijitolea kufanya shughuli hii na hali sema kwamba kabla ya kuwepo kwa vyama vingi kulikuwako na ofisi za CCM katika kila Balozi lakini baada ya kuingia kwa utawala wa vyama vingi ndipo serikali ilipoona ni vema kuacha balozi kubakia shughuli za kiserkali pekee, kwa hiyo amefurahishwa kuona wana CCM wa London wametafuta jinsi ya kukutana pamoja na kwamba CCM taifa itakuwa itashirikiana na tawi hili na kuleta taarifa za mara kwa mara ya yale yote yanayoendelea taifani.

Shughuli hii ilihudhuriwa na baadhi ya mawaziri, wabunge, Balozi, wafadhili "Malinzi family", Naibu Meya wa Jimbo la Ilala, waandishi wa habari na wanachama kutoka pande kadhaa za UK ambao baadaya Mh.Rais kuaga akiwa tayari kuelkea Tanzania kuhudhuria mazungumzo katika ya CCM na CUF, wao walienda na shuhguli ya kuchukua kadi zao za chama. Taarifa iliyosomwa na m/kiti wa tawi imeeleza kuwa mpaka sasa tawi hili lina wajumbe waliokwisha jiandikisha zaidi ya themanini(80) na kati ya hao walikwisha lipia kadi zao ni arobaini na mbili(42), kumi(10) wakiwa ni wanawake. Kadi inauzwa paundi tatu(£3) za mwingereza na ada ya uanachama ni paundi moja(£1) ya mwingereza kwa kila mwezi.

Monday 15 January 2007

Hatimaye Mh.J.K akutana na wananchi wake UK!

Baada ya subira waliokuwa nayo watanzania waishio Uingereza kwa zaidi ya miezi kumi na mitatu wakingojea kwa hamu kukutana na Rais wao Jamhuri ya Muungano wa awamu ya nne, Mh. Jakaya Mrisho Kikwete, hatimaye kiu hiyo ilipunguzwa kama si kukatwa kabisa siku ya jumapili ya tarehe 14 Januari 2007, pale Mh. J.K alipokutana na wananchi hawa katika Ukumbi wa Hotel ya Churchill katikati ya jiji la London. Mh.Rais wa Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania alikaribishwa ukumbini hapo kwa nyimbo na vigelegele.

Mkutano huo uliokuwa ukiratibiwa na ubalozi wa Tanzania nchi UK chini ya Mama Radhia Msuya ambaye alianza kwa kutoa ratiba nzima ya mkutano huo na kuwaomba radhi watanzania waliofika kukutana na rais wao mpya ambao walikuwa ni wengi mno kupelekea kukosa mahali pa kukaa na wengine wengi kushindwa kabisa kuingia ukumbini hapo, na ndipo baadaye Mh. Rais pamoja na msafara wake walipoingoa ukumbini hapo. Mama Msuya alimkaribisha rasmi M/kiti wa muda wa Tanzania Association (TA)UK, Bi Nora Sumari kusoma risala ambayo ilikuwa imeandawaliwa kiufasaha kabisa, na baadaye balozi alimkaribisha Mh.Rais kutoa hotuba kabla ya kipindi cha maswali na majibu ambacho hakikupata nafasi kutokana na ufinyu wa muda na ndipo Mh. Rais alipoomba radhi na kuwaahidi watanzania hao kwamba wakutane naye tena tarehe 17 Februari 2007 kwa kipindi cha maswali na majibu tu, na wananchi waliridhika na kukubaliana na ombi hilo.

Baada ya Rais kumaliza hotuba yake na kutokana na majukumu mengine ilibidi aage na kuacha mkutanoo ukiendelea kama ratiba ilivyopangwa kwa kuwakaribisha mawakala wa CRDB bank kuzungumza na watanzania juu akunti ya Tanzanite inayomwezesha mteja aishiye nje ya nchi kufungua akaunti, kuweka na kuchukua fedha Tanzania akiwa nje ya nchi, huduma ambayo watanzania wengi waishio nje ya nchi wamekuwa na hamu nao sana kwa kipindi kirefu. Na baada ya kuwasikiliza wamakala wa CRDB bank, watanzania wachache waliobaki ukimbini hapo waliendelea kufaidika kwa kupata maelezo ya kiutaalamu juu ya maswala ya kiuchumi na uwekezaji nchini Tanzania, maalezo hayo yalitolewa na wakuu wa TIC www.tic.co.tz tembelea tovuti hii ukipenda kujua zaidi. Pia watu walipata nafasi ya kuuliza na kujibiwa maswali yao mengi juu ya mambo ya uchumi na uwekezaji nchini Tanzania.

Msafara wa Rais ulikuwa ni pamoja na baadhi ya mawaziri, wabunge baadhi yao wakiwa ni wabunge kutoka kambi za upinzani CUF, wafanya biashara zaidi ya arobaini(40)na bila kumsahau mke wa Rais Bi. Salma Kikwete, ambaye naye baadaye alikuwa ameandaliwa hafla na chama cha wanawake UK, TAWA kinachoongozwa na Bi Mariamu Kilumanga.

Mh.Rais ameendelea kuwasisitiza watanzania walio nje ya nchi kurudi nyumbani mara wamalizapo shughuli zilizowaleta huku, wasiogope! Watanzania wameelezwa mabadiliko yanayoendelea kwa kasi nchini hasa kiuchumi, kijamii, kielimu, kimichezo na hata katika siasa na kwamba chachu yao inahitajika sana kusaidia kuongeza kasi hii ya maendeleo na wakwamba wasibakie kunung'unikia wageni bali waitangaze nchi yao mahali walipo duniani kote.

Ni matumaini yangu kuwa mmiminiko wa Tanzania waishio Uingereza na nchi nyingine za nje kurudi kuijenga nchi yao kwa kipindi cha miaka miwili ijayo itakuwa ni kasi ya ajabu mno.

Kwa habari zaidi na picha za tukio hili tafadhali tembelea www.tzuk.net

"Ni Mwaka Mpya, Nguvu Mpya, Ari Mpya, Kasi Mpya na Mambo Mapya"

CCM London- Swala la kihistoria!

Jumamosi ya tarehe 13 Jan 2007, saa 8 mchana (GMT) chama cha mapinduzi(CCM) ambacho ndicho chama tawala cha Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania kilifungua rasmi tawi la CCM katika jiji la London. Hili ni tawi la kwanza kabisa la chama cha mapinduzi nje ya nchi na mmoja wa jumbe walioshiriki katika shughuli za ufunguzi ambazo zilifanyika katika Hotel ya Holiday Inn- Brent Cross kaskazini ya mji wa London, ndugu Alan kalinga kutoka Reading alikaririwa akisema kwamba tawi hili ndilo litakalokuwa tawi tajiri kati ya matawi yote ya CCM, yetu macho na masikio.

Mwenyekiti wa muda wa tawi hili ndugu Maajar alifungua mkutano huu rasmi kwa kutoa habari kamili za hatua zote ambazo zimekwisha kuchuliwa na uongozi huo wa muda kuhakikisha swala hili linafanikiwa na si kuishia kuwa porojo/ndoto zisizotimilika miongoni mwa watanzania waishio Uingereza wenye imani na chama chao na ambao kwa muda mrefu sana wamekuwa wakifikiria ni jinsi gani ya kufanikisha jambo hili. Mwenyekiti huyo wa muda alieleza bayana hatua zote za awali za ufunguzi wa tawi alizozipitia ambazo ni kuanzia kuandika barua ya maombi ya kufungua tawi kwa wakuu wa chama hadi kufikia kuitisha mkutano huo na kuandikisha wanachama na tawi kukubalika na kutambulikana rasmi na uongozi wa juu wa chama. Mwenyekiti alifanikiwa kuonana na viongozi wengi wa juu wa chama kama si wote, kuzungumza nao na kupewa baraka zote. Viongozi hao ni pamoja na katibu mkuu wa CCM , Mh. Yusuf Makamba, Mwenyekiti wa CCM taifa Mh. John Malecela, Spika wa Bunge- Mh. Samwel Sitta na wengine wengi ambao alitaja kwa majina.
Pia m/kiti alifanikiwa kupata wafadhili wa tawi ni ambao ni pamoja na Bwana Jamal Malinzi mfanyibiashara maarufu nchini Tanzania ambaye alihudhuria katika ufunguzi wa tawi akiwa pamoja na msafara wake. Ama kwa hakika wajumbe wote waliodhuria mkutano huu walikiri kwamba kazi aliyoifanya mwenyekiti wa muda ndugu Maajar na Uongozi mzima wa muda unastahili pongezi nyingi mno.

Baada ya maelezo haya yote kutoka kwa M/kiti wa muda na baada ya wafadhili na wiongzi wengine walikuwa meza kuu kuongea ikiwa ni pamoja na Meya wa jimbo la Ilala ambaye naye pia alikuwapo katika shughuli hizi, wajumbe nao walipewa nafasi ya kuchangia mawazo. Kwa kuwa ilionekana kuwa karibu nusu ya wajumbe walioudhuria mkutanoni ilikuwa ni watanzania washio Reading, mjumbe Juma Pinto ambaye ndiye alikuwa mratibu wa shughuli nzima akishirikiana na kaka Abu Faraji, mjumbe aliomba kwamba kikao kitakachofuata cha tawi kifanye katika mji wa Reading ambako ni wazi kwamba kuna watanzania halisi wengi na pengine ambao ni wanachama wa chama cha CCM. Hili linaweza kuwa na ukweli ndani yake maana mji wa Reading ulitoa zaidi ya wagombea ubunge zaidi ya watano katika uchaguzi uliopita wengi wao kupitia tiketi ya chama tawala kama ndugu Maina Owino ambaye alikuwa akigombea nafasi na Mh. Pro Sarungi,na wengine kadhaa.

Kwa habari zaidi na picha za tukio hili la kihistoria tembelea www.tzuk.net au ukipenda kujua zaidi jinsi ya kujiandikisha kujiunga na CCM wasiliana nami kwa barua pepe.