Monday 15 January 2007

CCM London- Swala la kihistoria!

Jumamosi ya tarehe 13 Jan 2007, saa 8 mchana (GMT) chama cha mapinduzi(CCM) ambacho ndicho chama tawala cha Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania kilifungua rasmi tawi la CCM katika jiji la London. Hili ni tawi la kwanza kabisa la chama cha mapinduzi nje ya nchi na mmoja wa jumbe walioshiriki katika shughuli za ufunguzi ambazo zilifanyika katika Hotel ya Holiday Inn- Brent Cross kaskazini ya mji wa London, ndugu Alan kalinga kutoka Reading alikaririwa akisema kwamba tawi hili ndilo litakalokuwa tawi tajiri kati ya matawi yote ya CCM, yetu macho na masikio.

Mwenyekiti wa muda wa tawi hili ndugu Maajar alifungua mkutano huu rasmi kwa kutoa habari kamili za hatua zote ambazo zimekwisha kuchuliwa na uongozi huo wa muda kuhakikisha swala hili linafanikiwa na si kuishia kuwa porojo/ndoto zisizotimilika miongoni mwa watanzania waishio Uingereza wenye imani na chama chao na ambao kwa muda mrefu sana wamekuwa wakifikiria ni jinsi gani ya kufanikisha jambo hili. Mwenyekiti huyo wa muda alieleza bayana hatua zote za awali za ufunguzi wa tawi alizozipitia ambazo ni kuanzia kuandika barua ya maombi ya kufungua tawi kwa wakuu wa chama hadi kufikia kuitisha mkutano huo na kuandikisha wanachama na tawi kukubalika na kutambulikana rasmi na uongozi wa juu wa chama. Mwenyekiti alifanikiwa kuonana na viongozi wengi wa juu wa chama kama si wote, kuzungumza nao na kupewa baraka zote. Viongozi hao ni pamoja na katibu mkuu wa CCM , Mh. Yusuf Makamba, Mwenyekiti wa CCM taifa Mh. John Malecela, Spika wa Bunge- Mh. Samwel Sitta na wengine wengi ambao alitaja kwa majina.
Pia m/kiti alifanikiwa kupata wafadhili wa tawi ni ambao ni pamoja na Bwana Jamal Malinzi mfanyibiashara maarufu nchini Tanzania ambaye alihudhuria katika ufunguzi wa tawi akiwa pamoja na msafara wake. Ama kwa hakika wajumbe wote waliodhuria mkutano huu walikiri kwamba kazi aliyoifanya mwenyekiti wa muda ndugu Maajar na Uongozi mzima wa muda unastahili pongezi nyingi mno.

Baada ya maelezo haya yote kutoka kwa M/kiti wa muda na baada ya wafadhili na wiongzi wengine walikuwa meza kuu kuongea ikiwa ni pamoja na Meya wa jimbo la Ilala ambaye naye pia alikuwapo katika shughuli hizi, wajumbe nao walipewa nafasi ya kuchangia mawazo. Kwa kuwa ilionekana kuwa karibu nusu ya wajumbe walioudhuria mkutanoni ilikuwa ni watanzania washio Reading, mjumbe Juma Pinto ambaye ndiye alikuwa mratibu wa shughuli nzima akishirikiana na kaka Abu Faraji, mjumbe aliomba kwamba kikao kitakachofuata cha tawi kifanye katika mji wa Reading ambako ni wazi kwamba kuna watanzania halisi wengi na pengine ambao ni wanachama wa chama cha CCM. Hili linaweza kuwa na ukweli ndani yake maana mji wa Reading ulitoa zaidi ya wagombea ubunge zaidi ya watano katika uchaguzi uliopita wengi wao kupitia tiketi ya chama tawala kama ndugu Maina Owino ambaye alikuwa akigombea nafasi na Mh. Pro Sarungi,na wengine kadhaa.

Kwa habari zaidi na picha za tukio hili la kihistoria tembelea www.tzuk.net au ukipenda kujua zaidi jinsi ya kujiandikisha kujiunga na CCM wasiliana nami kwa barua pepe.

No comments: