Monday 15 January 2007

Hatimaye Mh.J.K akutana na wananchi wake UK!

Baada ya subira waliokuwa nayo watanzania waishio Uingereza kwa zaidi ya miezi kumi na mitatu wakingojea kwa hamu kukutana na Rais wao Jamhuri ya Muungano wa awamu ya nne, Mh. Jakaya Mrisho Kikwete, hatimaye kiu hiyo ilipunguzwa kama si kukatwa kabisa siku ya jumapili ya tarehe 14 Januari 2007, pale Mh. J.K alipokutana na wananchi hawa katika Ukumbi wa Hotel ya Churchill katikati ya jiji la London. Mh.Rais wa Jamuhuri ya Muungano ya Tanzania alikaribishwa ukumbini hapo kwa nyimbo na vigelegele.

Mkutano huo uliokuwa ukiratibiwa na ubalozi wa Tanzania nchi UK chini ya Mama Radhia Msuya ambaye alianza kwa kutoa ratiba nzima ya mkutano huo na kuwaomba radhi watanzania waliofika kukutana na rais wao mpya ambao walikuwa ni wengi mno kupelekea kukosa mahali pa kukaa na wengine wengi kushindwa kabisa kuingia ukumbini hapo, na ndipo baadaye Mh. Rais pamoja na msafara wake walipoingoa ukumbini hapo. Mama Msuya alimkaribisha rasmi M/kiti wa muda wa Tanzania Association (TA)UK, Bi Nora Sumari kusoma risala ambayo ilikuwa imeandawaliwa kiufasaha kabisa, na baadaye balozi alimkaribisha Mh.Rais kutoa hotuba kabla ya kipindi cha maswali na majibu ambacho hakikupata nafasi kutokana na ufinyu wa muda na ndipo Mh. Rais alipoomba radhi na kuwaahidi watanzania hao kwamba wakutane naye tena tarehe 17 Februari 2007 kwa kipindi cha maswali na majibu tu, na wananchi waliridhika na kukubaliana na ombi hilo.

Baada ya Rais kumaliza hotuba yake na kutokana na majukumu mengine ilibidi aage na kuacha mkutanoo ukiendelea kama ratiba ilivyopangwa kwa kuwakaribisha mawakala wa CRDB bank kuzungumza na watanzania juu akunti ya Tanzanite inayomwezesha mteja aishiye nje ya nchi kufungua akaunti, kuweka na kuchukua fedha Tanzania akiwa nje ya nchi, huduma ambayo watanzania wengi waishio nje ya nchi wamekuwa na hamu nao sana kwa kipindi kirefu. Na baada ya kuwasikiliza wamakala wa CRDB bank, watanzania wachache waliobaki ukimbini hapo waliendelea kufaidika kwa kupata maelezo ya kiutaalamu juu ya maswala ya kiuchumi na uwekezaji nchini Tanzania, maalezo hayo yalitolewa na wakuu wa TIC www.tic.co.tz tembelea tovuti hii ukipenda kujua zaidi. Pia watu walipata nafasi ya kuuliza na kujibiwa maswali yao mengi juu ya mambo ya uchumi na uwekezaji nchini Tanzania.

Msafara wa Rais ulikuwa ni pamoja na baadhi ya mawaziri, wabunge baadhi yao wakiwa ni wabunge kutoka kambi za upinzani CUF, wafanya biashara zaidi ya arobaini(40)na bila kumsahau mke wa Rais Bi. Salma Kikwete, ambaye naye baadaye alikuwa ameandaliwa hafla na chama cha wanawake UK, TAWA kinachoongozwa na Bi Mariamu Kilumanga.

Mh.Rais ameendelea kuwasisitiza watanzania walio nje ya nchi kurudi nyumbani mara wamalizapo shughuli zilizowaleta huku, wasiogope! Watanzania wameelezwa mabadiliko yanayoendelea kwa kasi nchini hasa kiuchumi, kijamii, kielimu, kimichezo na hata katika siasa na kwamba chachu yao inahitajika sana kusaidia kuongeza kasi hii ya maendeleo na wakwamba wasibakie kunung'unikia wageni bali waitangaze nchi yao mahali walipo duniani kote.

Ni matumaini yangu kuwa mmiminiko wa Tanzania waishio Uingereza na nchi nyingine za nje kurudi kuijenga nchi yao kwa kipindi cha miaka miwili ijayo itakuwa ni kasi ya ajabu mno.

Kwa habari zaidi na picha za tukio hili tafadhali tembelea www.tzuk.net

"Ni Mwaka Mpya, Nguvu Mpya, Ari Mpya, Kasi Mpya na Mambo Mapya"

1 comment:

Anonymous said...

Manyerere,
Hiyo akaunti ya Tanzanite nimeitafuta kwenye tovuti ya CRDB. Nimeipata, ilikuwa imejificha kweli. Tovuti hii si rafiki ya watumiaji hata kidogo. Ningependelea wangekuwa na sehemu ya "FAQ" kuhusu Tanzanite. Maswali wanayokutana nayo wanapotembea sehemu mbalimbali kama walivyokuja hapo wangeyakusanya na kuyaweka wazi na majibu yake ili wale ambao hatukuhudhuria tufaidike. Ndio faida ya teknolojia hizi.

Asante kwa kutupa habari za ziara ya Kikwete hapo Uingereza.